Nenda kwa yaliyomo

Mamluki

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Mike Hoare, aliyekuwa mamluki katika mgogoro wa kwanza wa Kongo.

Mamluki ni askari aliyekodiwa ambaye hayuko katika kikosi cha jeshi la nchi.[1] Mamluki hushiriki katika vita kwa ajili ya pesa au malipo mengine badala ya siasa au uzalendo.  

Neno la Kiswahili mamluki linatokana na Kiarabu مملوك mamlūk, kutoka kitenzi ملك "malaka" (sw. kumiliki), likimaanisha kiasili "anayemilikiwa". Kwa hiyo lilimtaja mtumwa na hasa mtumwa aliyeteuliwa kwa kazi ya uanajeshi. Kwa kawaida asili yao ilikuwa wavulana wadogo kutoka makabila wasio Waislamu, hasa Wakristo, waliochukuliwa kutoka kwa wazazi wao, kupewa mafundisho ya Uislamu na ya kijeshi, na kuingizwa katika vikosi maalumu.

Mamluki wa aina hii walitawala Misri ya Kiislamu kwa karne tatu, na Wajanisari wa Milki ya Osmani walikuwa mamluki waliohofiwa kote Ulaya.

Ilhali walitumiwa hasa nje ya nchi zao asili na mbali na familia zao, neno liliingizwa katika Kiswahili kwa maana ya "askari mgeni wa kukodiwa, mwenye asili ya nje".

Historia

[hariri | hariri chanzo]

Kwa jumla serikali nyingi walipendelea kutumia askari kutoka nje kwa sababu mbili:

  • kama shabaha ilikuwa kupambana na ghasia za ndani au uasi katika nchi yenyewe, askari wa nje walikuwa wepesi zaidi kutumia ukali dhidi ya wananchi kuliko askari wenyeji walioweza kukataa kuua ndugu zao
  • kama jeshi lilipaswa kupigania vita hatari ambako wengi wanaweza kufa, mara nyingi ni rahisi zaidi kupoteza wageni kuliko vijana wenyeji kwa sababu vifo vyao vinaweza kusababisha hasira ya wananchi, hasa kama vita ilienda vibaya

Afrika ya Kale

[hariri | hariri chanzo]

Katika Misri ya Kale, Farao Ramesses II aliwatumia mamluki 11,000 katika vita. Medjay, wanajeshi wa kukodiwa kutoka Nubia, walihudumu pamoja na jeshi la Misri wakati wa Ufalme wa Kale wa Misri hadi Ufalme Mpya wa Misri. Wapiganaji wengine walioajiriwa kutoka nje ya mipaka ya Misri ni pamoja na vikosi vya Walibya, Wasiria na Wakanaani wakati wa Ufalme Mpya na Washardana kutoka Sardinia ambao huonekana na helmeti maalum katika michoro, kama walinzi wa Ramesses II.[2]

Watawala Wagiriki wa Misri ya Ptolemaio, walitumia mamluki Wakelti.[3]

Mji wa Karthago (leo nchini Tunisia) ulitegemea mamluki katika vita vyake.

Karne ya 19 na 20

[hariri | hariri chanzo]
Frederick Russell Burnham katika Afrika.
Mgogoro wa Kongo
[hariri | hariri chanzo]
Mamluki Wazungu wakipigana bega kwa bega na vikosi vya Wakongo, mwaka 1964

Mgogoro wa Kongo wa miaka 1960-1965 ulikuwa kipindi cha machafuko katika Jamhuri ya Kwanza ya Kongo ambayo iliundwa kwa kupewa uhuru na Ubelgiji ikakatizwa baada ya Joseph Mobutu kuchukua madaraka ya nchi kwa mabavu. Katika kipindi hicho, mamluki walitumiwa na baadhi ya vikundi katika mgogoro na wakati mwingine, walitumiwa na Walinzi wa amani wa UM.

Katika miaka 1960 na 1961, Mike Hoare alikuwa mamluki aliyekuwa akiongoza kitengo cha wanajeshi waliokuwa wakiongea Kiingereza, kilichokuwa kikiitwa "4 Commando", kilichokuwa Katanga, mkoa ambao ulikuwa unajaribu kujitenga na Kongo ili uwe nchi huru chini ya uongozi wa Moise Tshombe. Hoare aliandika matukio hayo katika kitabu chake, Road to Kalamata.[4]

Katika mwaka wa 1964 Tshombe (aliyekuwa Waziri Mkuu wa Kongo) alimwajiri Meja Hoare aongoze kitengo cha kijeshi kilichokuwa kikiitwa "5 Commando", kilichokuwa na wapiganaji 300, ambao wengi wao walikuwa wametoka Afrika Kusini. Lengo la 5 Commando lilikuwa kupigana na kikundi cha waasi, kilichokuwa kikiitwa Simba, ambacho kilikuwa kimetwaa karibu thuluthi mbili za nchi.

Katika Operesheni Dragon Rouge, 5 Commando walishirikiana na wanajeshi Wabelgiji, marubani kutoka Kuba waliokuwa uhamishoni, na mamluki waliokuwa wameajiriwa na CIA. Lengo la Operesheni Dragon Rouge lilikuwa kutwaa Stanleyville na kuokoa mamia ya raia (hasa Wazungu na wamisionari) ambao walikuwa mateka wa waasi wa Simba. Operesheni hiyo iliokoa uhai wa watu wengi;[5] hata hivyo, ilimchafulia sifa Moise Tshombe kwa kuwa iliwarudisha mamluki Wazungu katika Kongo tu baada ya uhuru wa nchi. Ilikuwa mojawapo ya sababu za Tshombe kukosa msaada kutoka rais wa Kongo, Joseph Kasa-Vubu, ambaye alimpiga kalamu.

Wakati huo huo, Bob Denard aliongoza "6 Commando" na "Black Jack" Schramme aliamuru "10 Commando" na William "Rip" Robertson aliongoza kikosi cha Wakuba waliokuwa uhamishoni.[6]

Mamluki walitumiwa kupigana katika vita vya wenyewe kwa wenyewe Nijeria, miaka 1967-1970.[7] Wengine walitumiwa kuendesha ndege kwa niaba ya Wabiafra. Kwa mfano, Oktoba mwaka 1966, ndege aina DC-4M Argonaut ya shirika la ndege la Burundi lililokuwa likiendeshwa na mamluki Heinrich Wartski, aliyejulikana pia kama Henry Wharton, lilianguka Kameruni likiwa na bidhaa za kijeshi zilizokuwa zikipelekwa Biafra.[8]

Mei mwaka 1969, Carl Gustaf von Rosen aliunda kikosi cha ndege tano zilizokuwa zinajulikana kama Watoto wa Biafra (ing: Babies of Biafra) zilizoshambulia na kuharibu ndege za Nijeria[9] na kusambaza msaada wa chakula

Eritrea na Ethiopia
[hariri | hariri chanzo]

Nchi zote mbili ziliajiri mamluki katika Vita vya Eritrea na Ethiopia vilivyokuwa kati ya mwaka 1998 hadi 2000. Iliaminiwa kuwa mamluki kutoka Urusi walikuwa wakiendesha ndege za kivita za pande zote mbili.[10][11]

  1. "Protocol Additional to the Geneva Conventions of 12 August 1949, and relating to the Protection of Victims of International Armed Conflicts (Protocol 1), Article 47". International Committee of the Red Cross. Iliwekwa mnamo 20 Apr 2018.{{cite web}}: CS1 maint: date auto-translated (link)
  2. Healy, Mark; New Kingdom Egypt;
  3. "Rootsweb: Celts in Egypt". Archiver.rootsweb.ancestry.com. 24 Februari 2004. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2011-11-03. Iliwekwa mnamo 17 Oktoba 2011.{{cite web}}: CS1 maint: date auto-translated (link)
  4. Mike., Hoare, (2008). The road to Kalamata : a Congo mercenary's personal memoir (tol. la Paladin ed). Boulder, Colo.: Paladin Press. ISBN 9781581606416. OCLC 244068905. {{cite book}}: |edition= has extra text (help)CS1 maint: extra punctuation (link) CS1 maint: multiple names: authors list (link)
  5. "Changing Guard", Time Magazine, 19 December 1965. Retrieved on 6 June 2007. Archived from the original on 2007-09-30. 
  6. p.85 Villafaña, Frank Cold war in the Congo: The Confrontation of Cuban military forces, 1960–1967 Transaction Books
  7. The Mercenaries Archived 28 Mei 2013 at the Wayback Machine. in Time Magazine 25 October 1968
  8. Tom Cooper Civil War in Nigeria (Biafra), 1967–1970 13 November 2003. Second paragraph.
  9. Gary Brecher. Biafra: Killer Cessnas and Crazy Swedes Archived 14 Januari 2008 at the Wayback Machine 15 October 2004.
  10. "Sentinel Security Assessment - North Africa, Air force (Eritrea), Air force", Jane's Information Group, 26 October 2011. 
  11. Africa News Online: "In defiance, Eritrea was born; in defiance, it will live forever." 30 May 2000.